2 Kings 23:1-6

Yosia Analifanya Upya Agano

(2 Nyakati 34:3-7, 29-33)

1Kisha mfalme akawaita pamoja wazee wote wa Yuda na Yerusalemu. 2 aAkapanda kwenda hekaluni mwa Bwana pamoja na watu wa Yuda, watu wa Yerusalemu, makuhani na manabii, watu wote wakubwa kwa wadogo. Akasoma wakiwa wanasikia maneno yote ya Kitabu cha Agano, ambacho kilikuwa kimepatikana katika Hekalu la Bwana. 3 bMfalme akasimama karibu na nguzo, na kufanya upya agano mbele za Bwana: yaani kumfuata Bwana na kuzishika amri zake, maagizo na sheria kwa moyo wake wote na kwa roho yake yote, hivyo kuyathibitisha maneno ya agano yaliyoandikwa katika kitabu hiki. Kisha watu wote wakajifunga wenyewe kwa kiapo katika agano.

4Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani mkuu, makuhani waliomfuata kwa cheo, na mabawabu kuondoa kutoka kwenye Hekalu la Bwana vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali na Ashera na jeshi lote la mianga ya angani! Akavichoma nje ya Yerusalemu katika mashamba ya Bonde la Kidroni, na kuyachukua hayo majivu mpaka Betheli. 5 cAkawafukuza makuhani wa kipagani waliokuwa wameteuliwa na wafalme wa Yuda kufukiza uvumba katika mahali pa juu pa kuabudia miungu katika miji ya Yuda na ile iliyozunguka Yerusalemu, yaani wale waliofukiza uvumba kwa Baali, kwa jua na mwezi, kwa makundi ya nyota, na jeshi lote la angani. 6 dAkaiondoa nguzo ya Ashera kutoka kwenye Hekalu la Bwana, na kuipeleka kwenye Bonde la Kidroni nje ya Yerusalemu, akaiteketeza huko. Akaisaga hadi ikawa unga na kusambaza hilo vumbi juu ya makaburi ya watu wa kawaida.
Copyright information for SwhKC